Wabunge sharti waitwe ‘Waheshimiwa’ Kenya


image

Bunge la Kenya
Wakenya wanakabiliwa na tisho la kufungwa jela
mwaka mmoja au kulipa faini ya dola 23,000 kwa
kukosa kumuita mbunge ‘mheshimiwa’
unapozungumza naye.
Sheria hii mpya inayopendekezwa na wabunge wa
Kenya inalenga kuhakikisha kila afisaa mkuu wa serikali
anapewa heshima anayostahili.
Watakaovunja sheria hiyo watapata adhabu kali.
Adhabu hiyo itawakuta wale watakaokosa kumpa Rais
heshima zake kwa kumuita ‘Mtukufu Rais’, naye spika
wa bunge atapaswa kuitwa ‘Mheshimiwa spika wa
bunge’
Mswada huu uliwasilishwa na mbunge mmoja kwa jina
Adan Keynan, ambaye amesema kuwa umuhimu wake
ni kuonyesha heshima kwa maafisa wa serikali.
“ni muhimu kuonyesha picha nzuri ya nchi, kuhakikisha
kuna mpangilio na maadili mema katika mchakato wa
utawala, ” alisema bwana Keynan.
Huku mzozo kati ya wabunge na magavana ukiendelea
kutokota, mswada huo haujapendekeza chochote
kuhusu cheo cha magavana ambao ni wakuu wa
majimbo na watakavyoitwa.
Wataendelea kuitwa tu magavana.
Mswada huo pia unapendekeza kuwepo vyeo kwa
maafisa wa serikali kulingana na ukubwa wao.
Ikiwa mswada huo utakuwa sheria, cheo cha mbunge
kitakuwa juu zaidi kuliko cha gavana , majaji wa
mahakama ya juu , marais wa zamani na makamu wa
rais.
Kadhalika mswada huo utatumika katika kuweka
mpangilio kuhusu ambavyo maafisa wa serikali
watakuwa wanaketi katika hafla na mikutano ya
serikali.
Maafisa wa serikali watakaojipatia vyeo vingine mbali
na vile vitakavyoorodheshwa katika mswada huo
watatowa faini ya dola milioni mbili.