HII NDIO BAJETI YA 2014/15 :


image

Bunge la bajeti linaanza kesho
huku Serikali ikiwa imetoa
mwelekeo wa bajeti ya mwaka
wa fedha wa 2014/15 kuwa ni
Sh19.6 trilioni, ikilinganishwa na
Sh18.2 za Bajeti iliyopita.
Vipaumbele vya bajeti hiyo ni
kuendeleza Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano
ulioanza mwaka 2011 na Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN)
ambao unajumuisha maeneo sita
ya kitaifa ya kilimo, elimu, maji,
utafutaji wa rasilimali fedha,
nishati, uchukuzi na uboreshaji
wa mazingira ya kufanyia
biashara.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya, matumizi ya
kawaida kwa mwaka ujao wa
fedha yanalenga kufanikisha
mambo 20 muhimu, yakiwamo
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
mwaka 2014, Uchaguzi Mkuu
2015, kukamilisha mchakato wa
Katiba na nyongeza ya mishahara
na kulipa kwa wakati.
Waziri huyo alisema makadirio ya
matumizi ya maendeleo ni Sh7.7
trilioni sawa na asilimia 39 ya
matumizi yote ya Serikali na kati
ya fedha hizo miradi ya
maendeleo imetengewa Sh5.4
trilioni sawa na asilimia 27 na
matumizi mengine ya maendeleo
ni Sh2.2 trilioni.
Pia alisema katika mwaka wa
fedha 2014/2015, Serikali
imekusudia kukopa Sh4.2 trilioni
kutoka vyanzo vya mapato vya
ndani na nje ili kuziba pengo la
mapato.
Serikali imetenga Sh5.4 trilioni
kwa ajili ya miradi ya maendeleo
na imeonyesha vipaumbele vyake
vikuu katika miradi hiyo ya
maendeleo ni kilimo, elimu, maji,
utafutaji wa rasilimali fedha,
nishati, uchukuzi na uboreshaji
wa mazingira ya kufanyia
biashara huku michezo
ikikosekana katika vipaumbele
hivyo.
Sisi tunaamini sekta ya michezo
ilistahili kuingizwa katika
vipaumbele vya Serikali katika
bajeti yake ya 2014/15 kwani
sekta hii ikitengewa fedha nyingi
na kuwekewa misingi imara ni
chanzo kikubwa cha mapato.
Tumeshuhudia katika nchi
mbalimbali duniani ambazo
Serikali zao zinaithamini sekta ya
michezo kwa kuitengea bajeti
kubwa ya miradi ya maendeleo,
wanamichezo wa nchi hizo
wamekuwa wakinufaika na
kupata mapato makubwa na hivyo
kulipa kodi kubwa ambazo
zimekuwa ni chanzo kikubwa cha
mapato.
Ni wazi ukiangalia kwa undani
nchi zote zilizoendelea katika
michezo utaona kwa nanma moja
au nyingine kuna nguvu nyingi za
Serikali za nchi hizo hasa
utagundua Serikali za nchi zao
hutoa fedha na kuboresha
miundombinu ya michezo ili
kuweza kuwa na programu nzuri
za kuendeleza michezo na
husaidia timu zao za taifa.
Tunaamini kwamba hata kama
mapato ya nchi ni madogo,
Serikali ikiwa na dhamira ya
dhati ya kupenda michezo na
kuipa kipaumbele, haitashindwa
kupata vyanzo mbalimbali vya
mapato kwa ajili ya kuhakikisha
sekta ya michezo inakuwa katika
vipaumbele vya bajeti na
kutengewa fedha za kutosha kwa
ajili ya miradi ya maendeleo.
Inaeleweka kuwa Tanzania tuna
bahati ya pekee duniani kwani
tuna utajiri mkubwa wa rasilimali
ambazo kama kama zitatumika
ipasavyo zitanufaisha sana taifa
letu na wanamichezo wetu
watapata vifaa vya michezo kwa
bei nafuu, viwanja vya michezo
na walimu bora wa michezo.
Hata hivyo katika hali ya
kushangaza utajiri huo wa
rasilimali umekuwa ukionekana
kunufaisha wachache huku hali
hiyo ikionekana kama ni jambo la
kawaida. Tunatarajia wabunge
watatuunga mkono na kuisimamia
Serikali ipasavyo katika
kuhakikisha kuanzia Bunge hili la
bajeti sekta ya michezo
inatambuliwa na kutengewa
fedha nyingi katika miradi ya
maendeleo.(CHANZO:
MWANANCHI) (FS)