Kesi ya kutorosha Twiga: Mwandishi jela baada ya aliyemdhamini kutoroka


image

Moshi. Mwandishi wa habari wa siku
nyingi, Peter Temba amehukumiwa
kifungo cha miezi sita jela baada ya
kushindwa kumpeleka mahakamani
mshtakiwa aliyemdhamini katika kesi
ya kutorosha twiga kwenda Uarabuni.
Mwandishi huyo anayeandikia Gazeti
la
Serikali la Daily News na
mwenzake aliyekuwa akiandikia Gazeti
la Nipashe, Jackson Kimambo
walimdhamini mtuhumiwa huyo raia wa
Pakistan, Kamran Ahmed ambaye ni
mshtakiwa namba moja katika kesi
hiyo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa
Kilimanjaro ilitoa amri ya
kuwakamata wadhamini hao baada ya
mshtakiwa waliyemdhamini kwa kutia
saini hati ya dhamana ya maneno ya
(bond) ya Sh14.2 milioni, kutoroka.
Waandishi hao walimdhamini
mshitakiwa huyo Juni 11, 2011 baada
ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Moses Mzuna kuamuru kila mshtakiwa
akabidhi mahakamani Sh14.2 milioni
au mali yenye thamani hiyo.
Sharti la pili lilikuwa kila
mshtakiwa katika kesi hiyo ya
kutorosha twiga wanne na wanyama
wengine 148 kwenda Uarabuni, kuwa na
wadhamini wawili wakazi wa
Kilimanjaro watakaosaini dhamana ya
Sh14.2 milioni kila mmoja na
waliojitokeza ni waandishi hao.
Kesi hiyo ikiwa katika hatua za
usikilizwaji, Ahmed aliruka masharti
ya dhamana na kwa miezi takriban
mitano vyombo vya dola vimekuwa
vikimtafuta kwa udi na uvumba bila
mafanikio na hata wadhamini wake
walishindwa kumpeleka mahakamani
hadi ilipotolewa hati ya kuwakamata.
Temba alikamatwa Jumatatu wiki hii
na kufikishwa mahakamani mbele ya
Hakimu Mkazi wa Mkoa Mfawidhi, Simon
Kobelo na alipoulizwa alipo
mshtakiwa huyo alisema hajui na hana
Sh14.2 milioni alizosaini kama
dhamana.
Wakili wa Serikali, Stella Majaliwa
aliomba sheria ichukue mkondo wake
kwa kuwa mshtakiwa katika kesi hiyo
pamoja na mdhamini wa pili
hawajulikani walipo.
Kobelo alisema sheria iko wazi na
kwamba kulingana na Kifungu cha
160(4) cha Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai (CPA), kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka
2002, mdhamini huyo atatumikia
kifungo cha miezi sita jela.
Kufungwa kwa mwandishi huyo kumeibua
simanzi kubwa miongoni mwa
wanahabari na familia yake hasa
ikizingatiwa kuwa ni mwaka jana tu,
alikatwa mguu mmoja kutokana na
maradhi ya kisukari.
Chanzo: Mwananchi