Mlipuko waua 21 na kujeruhi 50 Nigeria


image

Moto ukiteketea kulikolipuka bomu nje ya kituo cha
biashara Abuja, Nigeria.
Kumetokea shambulizi la bomu mbele ya soko
lenye shughuli nyingi katika mji mkuu wa Nigeria
Abuja na kuwauwa zaidi ya watu 21.
Taswira ya
majonzi na kilio ilitanda katika mji wa
Abuja, mamia ya watu waliokuwa wakinunua bidhaa
katika soko hilo wakijikuta wakivuja damu kutokana
na majeraha ya mlipuko huo na wengine kuishia
mauti.
Bomu hilo lililipuka mbele ya kituo kikubwa cha
biashara, kinachotembelewa na watu wengi.
Walioshuhudia walisema sehemu za miili ya
wanadamu zilitapakaa kila mahali sakafuni.
Magari yalichomeka kabisa na vioo katika
madirisha ya nyumba zilizokuwa karibu kuvunjika
vyote. Watu waliokuwa na hofu walielekea kwenye
mahospitali yaliyo karibu ambapo walishuhudia
magari ya wagonjwa yakisongamana kila mahali
yakiwaleta wagonjwa na miili ya waliokufa.
John Tobi Wojioa aliwasili mahali hapo muda mfupi
baadaye akimtafuta jamaa wake. Alitaja alichoona
kama mafuriko ya damu:
“Kulikuwepo magari ya wagonjwa wa shirika la
FRCS (federal Road Safery Corps) na ya mashirika
mengine yaliyokuwa yakiingia na kuondoka
yakibeba miili ya waathirika. Kwenye barabara
alama za damu za nyayo za wanadamu zilionekana
kila mahali,” alisema Bwana Wojioa.
Bahati kwa Bwana Wojioa ni kuwa jamaa wake
baadaye alipatikana akiwa hai huku akiendelea
kutulia kutokana na mlipuko huo.
Hii ni mara ya tatu kwa mji mkuu kulengwa na
milipuko tangu Aprili. Kundi la Waismalu waenye
itikadi kali la Boko Haramu lilidai kuhusika katika
milipuko mbili ya awali ambako zaidi ya watu 90
walifariki.
Milipuko hiyo ilitokea kando mwa jiji lakini huu wa
sasa umetokea katikati mwa jiji katika Wilaya ya
Wuse 2 na hofu yake itatanda katika mji wote.
Kwa mara nyingine tena Boko Haram watashukiwa
kuhusika katika mlipuko huu. Kundi hilo limelipua
miji kadhaa nchini Nigeria huku likiendesha
kampeni yake ya kuwashambulia raia katika
maeneo ya mashambani hasa Kaskazini Mashariki
mwa taifa hilo.
Mnamo Jumanne watu waliokuwa wakitoroka vijiji
katika jimbo la Borno walisema kuwa makumi ya
wanawake na watoto walikuwa wametekwa nyara.
Lakini Serikali kwa upande wake ikasema kuwa
hakuna ushahidi kuwa utekaji nyara ulitendeka.
Serikali ilisema vivyo hivyo wakati zaidi ya
wasichana wanafunzi zaidi ya 200 walitekwa nyara
na Boko Haram mnamo Aprili.
Wachunguzi wengi wanasema kuwa kwa
kukanusha kuwa kuna utovu wa usalama nchini
Nigeria, Serikali imechanganyikiwa kwa sababu
milipuko ya mabomu ya mara kwa mara ni ushahidi
tosha kuwa ukosefu wa usalama ndio ukweli wa
mambo nchini.